Tuesday 12 June 2012

SAITOTI NA OJODE WAFARIKI AJALINI




KENYA imegubikwa na wingu jeusi baada ya maafisa Waziri wa Usalama wa Ndani Profesa George Saitoti na Waziri Msaidizi Orwa Ojode kufariki kwenye ajali ya ndege, eneo la Ngong.
Wengine waliofariki kwenye ajali hiyo iliyotokea mwendo wa saa mbili na nusu asubuhi ni walinzi wao wawili na marubani wawili.
Ajali hiyo ilitokea walipokuwa wakielekea katika eneo la bunge la Ndhiwa, alilowakilisha Bw Ojode, kuhuhuria ibada ya Jumapili, na baadaye kuongoza sherehe ya kuchangisha pesa.
Ndege hiyo aina ya Helikopta AS 350 ya idara ya polisi, ilianguka dakika chache baada ya kuondoka uwanja wa Ndege wa Wilson, kilomita moja kutoka barabara ya Nairobi - Ngong, eneo la Kibiku, ndani ya msitu wa Ngong.
Walioshuhudia ajali  hiyo walisema Ndege ilianguka kwa kishindo kabla ya kulipuka na kuwaka moto.
Abiria wote walichomeka kiasi cha kutotambuliwa huku bidhaa zao za kibinafsi na bastola za walinzi zikitapakaa eneo la mkasa.
Mabaki ya ndege hiyo iliyoharibika kabisa, pia yalitawanyika katika eneo hilo.
Maafisa wa kijeshi na polisi walifika na kuzuia wananchi kukaribia eneo la mkasa, huku wakikusanya habari za  kusaidia katika uchunguzi.
Kilichosababisha ajali hiyo hakikujulikana mara moja.
Polisi waliondoa miili sita iliyochomeka vibaya katika eneo la mkasa na kuipeleka katika Mochari ya Lee Funeral home. Idara ya Habari ya Rais ilisema walinzi waliokufa ni Inspekta Joshua Tonkei na Sajini Thomas Murimi, nao marubani ni Luke Oyugi na  Nancy Gituanja wa kikosi cha polisi.
Risala za rambirambi
Rais Mwai Kibaki na Waziri Mkuu Raila Odinga waliongoza maafisa wakuu wa Serikali kuomboleza maafisa hao na kutumia  familia zao risala za rambirambi.
Kwenye risala yake, Rais Kibaki alisema alihuzunishwa na kifo cha Profesa Saitoti na Bw Orwa Ojode, walinzi wao na marubani wa ndege hiyo.
“Vifo vyao ni pigo kubwa kwa taifa hili,” Rais Kibaki alisema.
Alisema Profesa Saitoti, atakumbukwa daima kwa kujitolea kuwahudumia Wakenya. Alikumbuka jinsi Profesa Saitoti alihutubia mkutano wa kuandaa mikakati ya amani wakati wa uchaguzi mkuu mjini Mombasa wiki jana.
Bw Odinga na Makamu wa Rais Kalonzo Musyoka walikuwa miongoni mwa maafisa wakuu wa Serikali kufika eneo la mkasa.
Bw Odinga alisema uchunguzi umeanzishwa kubaini chanzo cha ajali hiyo. “Tuungane katika kipindi hiki kigumu cha dhiki katika taifa letu,” Bw Odinga alisema.
Waziri Mkuu alifutilia mbali ratiba yake ya mwisho wa wiki kufuatia mkasa huo na kutembelea  eneo la mkasa.
Naibu Waziri Mkuu Musalia Mudavadi pia alifutilia mbali ziara yake ya kujipigia debe mkoani Rift Valley kufuatia mkasa huo.


Bw Kalonzo alitaja ajali hiyo kama mkasa wa kitaifa.
“Inasikitisha kupoteza Prof Saitoti na Bw Ojode. Vifo vyao ni pigo kwa nchi hii” Bw Musyoka alisema.
Maafisa wengine waliofika eneo hilo ni Spika wa Bunge Kenneth Marende na Kamishna wa Polisi  Bw Mathew Iteere.

No comments:

Post a Comment

Ji husishe kwa maoni yako ndio ukweli upatikane kwa manufaa wetu