Tuesday 12 June 2012

HUENDA KESI ZA ICC ZIANZE MACHI 2013


MAHAKAMA ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), Jumatatu iliashiria kuwa huenda kesi ya mashtaka dhidi ya washukiwa wanne wa ghasia za baada ya uchaguzi zikasikizwa baada ya uchaguzi mkuu ujao.
Upande wa mashtaka ulikubaliana na mawakili wa Mbunge wa Eldoret Kaskazini William Ruto na mtangazaji Joshua Sang kuwa kesi hizo zianze kusikizwa baada ya Machi 2013. Upande wa mashtaka ulisema utahitaji kipindi hicho kinachokamilika mwishoni mwa Machi ili kutoa ushahidi dhidi ya washukiwa hao wawili.



Bw Ruto na Bw Sang hata hivyo watasubiri hadi Julai 13 kujua wakati kamili kesi zao zitaanza kusikizwa. Jaji Kuniko Ozaki alitangaza hayo baada ya kusikiza upande wa mashtaka na utetezi kuhusiana na ni lini kesi hiyo ianze kusikizwa.
Katika kikao cha kwanza cha kutathmini jinsi kesi hizo zitaendeshwa, pande za mashtaka na ule unaowakilisha washtakiwa zilikubaliana na pendekezo kuwa kesi hizo zianze Machi mwaka ujao.
Mwakilishi wa upande wa mashtaka alisema iwapo kesi hizo zitasikizwa Machi 2013, washtakiwa watahitajika kuwasilisha nakala kuwa watahudhuria vikao vyote licha ya matokeo ya uchaguzi mkuu.
Hii ni kutokana na kuwa Mabw Uhuru Kenyatta na William Ruto wanatarajiwa kuwa wagombeanaji wa kiti cha Urais katika uchaguzi mkuu ujao.
Upande wa mashtaka pia ulitaka ukubaliwe kutoa majina ya mashahidi walio chini ya ulinzi wa mahakama siku 60 kabla ya kuanza kwa vikao, na siku 30 kwa mashahidi ambao hawako chini ya mpango huo.

Nakala za ushuhuda
Kutokana na hitaji la kulinda mashahidi, upande wa mahakama uliongeza kuwa utalazimika kuchelewesha kutoa nakala za ushuhuda.
Hata hivyo, Bw Katwa Kigen anayemwakilisha Bw Joshua Sang, alisema siku 30 ni chache, na akapendekeza muda huo uongezwe hadi siku 45.
Kwa upande wake, wakili wa Bw William Ruto, Bw John Hooper alisema kiwango cha jinsi usalama wa mashahidi unavyochukuliwa kuwa suala nyeti, huenda ukaathiri uchunguzi wa upande wa washtakiwa.
Hata hivyo, jopo la mahakimu liliamrisha kuwa nakala zinazoweza kutolewa bila kudhuru usalama wa mashahidi zikabidhiwe kwa washtakiwa haraka iwezekanavyo.
Jopo hilo pia liliamrisha pande zote mbili zikubaliane jinsi uhariri utafanywa kwenye nakala za mashtaka zitakazotumiwa, kabla tarehe tatu Julai.
Majaji wengine katika jopo hilo ni Christine Van den Wyngaert, raia wa Ubelgiji na Chile Eboe-Osuji wa Nigeria. Bi Ozaki ni raia wa Japan.
           
                                                                                                Kwa Hisani ya Swahili Hub.

No comments:

Post a Comment

Ji husishe kwa maoni yako ndio ukweli upatikane kwa manufaa wetu