HAKI KWA WASHUKIWA KUKIUKWA KULINGANA NA WAKILI WA UPANDE WA FAMILIA YA MARHEMU SHEIKH ABOUD ROGO
OMBI la polisi la kutaka kijana wa marehemu mhubiri wa Kiislamu Sheikh Aboud Rogo na wenzake sita kuzuiliwa katika kituo cha polisi limekubaliwa na mahakama Mombasa.
Hii ni baada ya mchunguzi wa kesi Daniel Makau kuiambia mahakama kwamba polisi walikuwa na habari za kuaminika kuwa kungekuwa na mashambulizi ya pamoja katika sehemu zisizotambulika katika miji ya Nairobi na Mombasa.
Katika cheti chake cha kuapa (affidavit), Bw Makau, alisema kuwa walipata habari ya kuwa kuna watu waliokuwa wanapanga kufanya vitendo vya kigaidi katika miji hiyo miwili.
Katika cheti hicho, Bw Makau alisema kuwa mabwana Swaleh Abdulmajit, Khubeib Aboud Rogo, Swaleh Ali alias Ronaldo, Bilal Gaitho, Juma Musa alias Chidi, Hashim Yassir na Mzee Suleiman wanahusika au wako na habari ambazo zinaweza kusaidia katika uchunguzi.
Hakimu mkaazi Bi Renee Kitagwa alikubali ombi la polisi la kutaka washukiwa kuzuiliwa kwa siku saba akisema kuwa suala hilo lilikuwa ni la umuhimu kwa umma.
Bw Makau alimwambia Bi Kitagwa kwamba uchunguzi utahitaji mienendo ya kati ya eneo la Pwani na sehemu nyingine za nchi.
Naomba mahakama kunipatia siku saba ili nimalize uchunguzi,”alisema Bw Makau.
Wakili wa washukiwa Francis Kadima aliambia mahakama kuwa mtoto wa marehemu Rogo alikamatwa wakati akiendelea na shugli za harusi ambazo hazijakamilika.
Bw Kadima alisema kuwa kuna umuhimu wa kuhakikishiwa kwamba siku saba zilizoombwa zikiisha hakutakuwa na maombi mengine ya muda zaidi.
“Wakati wote hawa saba walikuwa wamekamatwa bila kuwa na nafasi ya kuwasiliana na jamaa zao na wakili,” alisema Bw Kadima.
Bw Kadima aliisihi mahakama kuwaruhusu jamaa kuwaona na pia yeye ili aweze kupewa maagizo kamili.
Matibabu
Wakili huyo pia aliiambia mhakakama kuwa washtakiwa walikuwa wanahitaji matibabu na kwamba wanastahili kupelekwa katika hospitali kuu ya mkoa wa Pwani waangaliwe na daktari.
“Washukiwa wapatiwe dhamana kama uchunguzi haujakamilika kwa siku saba,”alisema Bw Kadima.
Hakimu ambaye alikataa kuweka kiwango cha siku ambacho washukiwa watazuiliwa rumande pia aliagiza kuwa washukiwa waruhusiwe kumwona wakili wao na wapelekwe hospitalini.
Inatarajiwa ya kuwa washukiwa watazuiliwa katika vituo vya polisi vya Makupa, Port, Railways na Central.
No comments:
Post a Comment
Ji husishe kwa maoni yako ndio ukweli upatikane kwa manufaa wetu