WAZIRI Msaidizi wa Usalama wa Ndani, Bw Orwa Ojode, alikuwa mwanasiasa wa kipekee na aliyeshangaza wengi kutokana na bidii yake kazini.
Amejulikana sana kutokana na alivyotetea Idara ya Polisi na wizara yake kwa jumla bungeni. Mara nyingi alilazimika kujibu maswali kwa niaba ya waziri wake.
Alichaguliwa bungeni kwa mara ya kwanza mwaka wa 1994 baada ya kujiondoa kwa aliyekuwa Mbunge wa Ndhiwa kupitia chama cha Kanu, Bw Tom Obondo.
Alichaguliwa tena kama Mbunge katika uchaguzi wa mwaka wa 1997 na 2002, kupitia chama cha National Development Party (NDP).
Mwaka wa 2007, alichaguliwa kuwakilisha eneo bunge hilo kupitia chama cha ODM.
Alikuwa na mpango wa kuwania kiti cha Seneta, kaunti ya Homa Bay, katika uchaguzi mkuu ujao.
Bw Ojode alikuwa kigogo wa kisiasa kutoka eneo la Nyanza, na rafiki wa karibu wa Waziri Mkuu Raila Odinga.
Hata hivyo, tabia yake ya kutoa maoni ya kibinafsi bila kusukumwa na hisia za wengine zilipelekea baadhi ya wanasiasa wa ODM kushuku kuwa alikuwa na uhusiano wa karibu na mahasimu wao.
Aliwahi kutofautiana na maoni ya Bw Odinga kuhusu kuachwa wazi kwa mipaka ya Kenya na Somalia ili kuruhusu wakimbizi waingie nchini.
Huku Waziri Mkuu akishikilia kuwa Kenya ilitakikana kusaidia wakimbizi kwani iko chini ya mkataba wa Umoja wa Mataifa, Bw Ojode alisisitiza kuwa usalama wa Wakenya ni muhimu zaidi, hivyo basi Wizara haingekubali kuwepo kwa hatari ya wanamgambo wa Al-Shabaab kuingia nchini.
Kutofautiana na chama
Hivi majuzi, alitofautiana na msimamo wa chama chake kutaka mazungumzo yafanywe na kundi la Mombasa Republican Council (MRC) kwa kusisitiza kundi hilo litazidi kuchukuliwa kama kundi haramu nchini.
Ukakamavu wake katika Wizara ilipelekea wafuasi wake kumbandika jina 'Sirkal’, kuwashiria alikuwa mwamuzi wa masuala ya usalama nchini.
Katika makao ya Bunge, alipongezwa mara kwa mara kwa kujizatiti kuhakikisha alifika bungeni kujibu maswali yaliyowasilishwa kwa Wizara yake.
Zaidi ya hayo, alichukua wajibu wa kutetea Mawaziri ambao hawangeweza kufika bungeni kujibu maswali.
Hapakuwa na pingamizi kuwa Bw Ojode alikuwa na mitindo ya kipekee kuunda urafiki wa karibu na watu wenye misimamo tofauti tofauti.
Hii ilidhihirika wakati wa mazishi ya babake, ambayo yalihudhuriwa na idadi kubwa ya wabunge, wakiongozwa na Rais Mwai Kibaki, Bw Odinga, Naibu Waziri Mkuu Uhuru Kenyatta na wafuasi wao.
No comments:
Post a Comment
Ji husishe kwa maoni yako ndio ukweli upatikane kwa manufaa wetu