Tuesday, 12 June 2012

KIFO KIMEZIMA NDOTO YA SAITOTI KUTAKA KUWA RAIS



KIFO cha Waziri wa Usalama Prof George Saitoti kimezima ndoto ya mmoja wa wanasiasa mashuhuri na aliyekuwa ametangaza nia ya kuwania urais.
Ni mwanasiasa aliyeingia kwenye siasa katika hali ambayo haikutarajiwa na kufanikiwa kwake hadi kuwa makamu wa rais kulishangaza wengi.
Kwenye siasa, alipanda na kushuka ingawa alibaki mwingi wa matumaini.
“Nimekuwa Makamu wa Rais kwa miaka 12. Waziri wa mipango miaka tisa, Waziri wa Fedha tano na Waziri wa Elimu miaka tano. Mimi ni Mwenyekiti wa chama cha PNU na mtu yeyote asiulize iwapo niko katika kinyang’anyiro au la,” alieleza mara nyingi akitangaza nia yake ya kutaka kuwa rais.
Hii sasa itabaki kuwa historia. Alijitosa kwenye siasa mwaka wa 1983 aliposhawishiwa na washirika wa kisiasa wa Rais mstaafu Daniel arap Moi wakati  alipokuwa Mhadhiri wa Hesabu katika Chuo Kikuu cha Nairobi, aliteuliwa moja kwa moja kama Mbunge maalum na Waziri wa Fedha.
Katika uchaguzi mkuu wa 1988 alishinda kiti cha ubunge cha Kajiado Kaskazini. Alichaguliwa tena mwaka wa 1992 na kuteuliwa kama Makamu wa Rais na Waziri wa Mipango na Ustawi wa Kiaifa.
Mwaka wa 1997 alihifadhi kiti chake cha ubunge na akarejeshewa uwaziri. Mwaka wa 1999 aliteuliwa tena kuwa Makamu wa rais. Kati ya mwaka wa 2001-2002 alihamishwa hadi Wizara ya Masuala ya Ndani huku akisalia kuwa Makamu wa Rais.
Uaminifu mkubwa
Ingawa alikuwa amehitimu katika daraja ya juu zaidi ya masomo , aliyatekeleza majukumu yake kwa uaminifu mkubwa kwa Rais Moi. Mara nyingi alikejeliwa lakini hakufa moyo. Wakati mmoja alipokonywa nyadhifa ya umakamu kwa kipindi cha miezi 14 na kisha kurejeshwa kwa tangazo lililofanyika barabarani.
Atakumbukwa kwa usemi wake “Wakati hufika ambapo taifa ni muhimu kuliko mtu binafsi.”
Baada ya kukosa kuidhinishwa na Rais mstaafu kuwania urais 2002, Saitoti alijiunga na viongozi wengine kubuni chama cha NARC ambacho kilishinda.
Baada ya Uchaguzi wa mwaka wa 2002 aliteuliwa Waziri wa Elimu ambapo alisimamia kuanzishwa kwa Mpango wa Elimu Bila Malipo shule za msingi.
Alisalia kuwa mshirika mkuu wa Rais Kibaki na hakupenda kujihusisha na matamshi ya kuzua mijadala.
Alikuwa na Shahada ya Sanaa, Shahada ya pili ya Sayansi na Shahada ya Usamili katika Isabaki kutoka vyuo vya Brandeist (Marekani), Sussex, Brighton na Warwick Uingereza mtawalia.
Alijiunga na Chuo Kikuu cha Nairobi kama mhadhiri mwaka wa 1972 ambapo alipanda cheo na akawa mwenyekiti Idara ya Isabaki Saitoti alihudumu katika nyadhifa hii hadi alipoteuliwa Makamu wa rais na Waziri wa Fedha mwaka wa 1989.
Katika nyanja ya usomi, Saitoti aliwahi kuhudumu katika nyadhifa mbali mbali kwa mfano alikuwa Naibu wa Rais wa Muungano wa Hesabu barani Afrika (1976-1979), Mwenyekiti wa Shirika la Fedha duniani na mwana chama wa Bunge la Afrika Mashariki.


                                                                                                                                 Kwa hisani ya Swahili Hub 

No comments:

Post a Comment

Ji husishe kwa maoni yako ndio ukweli upatikane kwa manufaa wetu