Friday, 23 November 2012

MWANAMUME ASHAMBULIWA NA KUJERUHIWA NA TUMBILI


John Mwangi
John Mwangi akiwa hospitalini Nyeri anakouguza majeraha baada ya kushambuliwa na tumbili kijiji cha Watuka, Kieni Magharibi. Picha/JOSEPH KANYI 
Na ERIC MUTAI
Mwanamume wa umri wa miaka 44 anauguza majeraha katika hospitali ya mkoa ya Nyeri baada ya kushambuliwa na tumbili katika kijiji cha Watuka wilayani Kieni Magharibi.

MWANAMUME wa miaka 44 anauguza majeraha katika hospitali ya mkoa ya Nyeri baada ya kushambuliwa na tumbili katika kijiji cha Watuka wilayani Kieni Magharibi.
John Mwangi alikuwa ameenda shambani mwake kulinda mimea yake dhidi ya kuharibiwa na tumbili kabla ya tukio hilo.
Akiongea na Taifa Leo katika kitanda hospitalini, baba huyo wa watoto wanne alisema kuwa tumbili mmoja mwenye mwili mnene alimshambulia alipojaribu kumfukuza kutoka shambani.
Alieleza kuwa aliwapata tumbili kadhaa wakisherehekea mimea yake ndipo alipoanza kuwapigia kelele na kuwafukuza akiwa ameandamana na mbwa wake.
Tumbili walitoroka kuelekea msitu mdogo ulio karibu na shamba lake lakini mmoja aliyekuwa mnene hakutoroka bali aliendelea kuangalia Bw Mwangi alivyokuwa akifanya bila kutishika.
“Nilimuangalia kwa muda kwani sikujua nia yake ndipo mbwa wangu akaanza kucheza naye. Nilienda kando kidogo kutafuta fimbo nimfukuze nayo ndipo akaruka mbele yangu na kunishika mikono,” alisema Bw Mwangi.
Tumbili huyo alianza kumuuma mikono Bw Mwangi aliyekuwa akipiga mayowe kwa uchungu aliokuwa anasikia.
Alisema aling’ang’ana lakini tumbili akamzidi nguvu na kumuangusha chini na kuanza kumuuma miguuni na kumkwaruza tumbo kwa kucha.
“Nilikuwa napiga kelele kwani nilihisi uchungu mwingi sana. Alipokuwa ananitafuna miguu nilimrushia teke moja lililompata kwa tumbo ndipo aliniwachilia na kukimbia. Sijawahi kuona wala kusikia jambo kama hilo maishani mwangu,” alisema Bw Mwangi.
Wanakijiji waliosikia mayowe walifika mahali pale kumsaidia na wakampata akiwa anatokwa na damu mikononi na miguuni lakini tumbili alikuwa amekwisha ondoka.
Kufanyiwa upasuaji
Walimkimbiza katika hospitali ya mkoa ya Nyeri alikopelekwa katika chumba cha upasuaji na kudungwa shindano ya kuzuia kuambukizwa ugonjwa.
Bw Mwangi alivunjika mkono wa kulia wakati alipokuwa waking’ang’ana na tumbili.
Alielezea kuwa wanaume hushinda kwenye mashamba wakilinda mimea yao isiharibiwe na tumbili ambao ni wengi katika sehemu hiyo.
Wakati mwingine wanakijiji huwaita maafisa wa wanyama pori (KWS) kuwaondoa tumbili na huwa wanawafukuza hadi katika msitu mdogo ulio karibu. Tumbili hurudi tena kushambulia mashamba maafisa hao wakiondoka.
“Tumbili hao huwa hawaogopi wanawake na watoto. Hata mwanamke afanye nini tumbili hawawezi kumuogopa. Ikiwa wanaweza kumshambulia mwanamume mzima kama mimi, tunashangaa wanaweza kuwafanya nini wanawake na watoto,” alisema Bw Mwangi.
Familia yake ilimtembelea hospitalini na kudai fidia kutoka kwa shirika la KWS, ikisema kuwa wanyama walimshambulia akiwa shambani mwake.
Waliomba wanyama hao waondolewe sehemu hiyo kwani wanasababisha hasara kubwa kwa kuharibu mimea yao .
Aidha wanasema wanahofia maisha yao baada ya kisa kilichompata Bw Mwangi.
Credits: Swahili Hub

No comments:

Post a Comment

Ji husishe kwa maoni yako ndio ukweli upatikane kwa manufaa wetu