Friday 23 November 2012

Demokrasia ya CCM TANZANIA imepita viwango vya kimataifa


TUMESHUHUDIA Mkutano Mkuu wa nane wa CCM ukimalizika kwa kuwapata viongozi wa juu wa chama hicho na kuhitimisha chaguzi zake za ndani zilizoanzia kuanzia ngazi ya shina hadi taifa.

Baada ya mkutano huo, chama hicho kupitia Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kimeunda Sekretarieti mpya iliyosheheni vigogo wanaotarajiwa kukivusha kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Pia mkutano huo umewachagua viongozi wa juu, akiwamo Mwenyekiti, Rais Jakaya Kikwete akisaidiwa na wenyeviti wawili, Philip Mangula wa Bara na Rais Ali Mohamed Shein wa Zanzibar.
Nafasi ya Katibu Mkuu amepewa Abdulrahman Kinana akisaidiwa na Mwigulu Nchemba (Bara) na Vuai Ali Vuai (Zanzibar).
Wajimbe wengine wa Sekretarieti ni Dk Asha Rose Migiro (Siasa na Uhusiano wa Kimataifa), Zakhia Meghji (Uchumi na Fedha), Mohamed Seif Khatib (Oganaizesheni) na Nape Nnauye anayeendelea na nafasi yake ya Itikadi na Uenezi.
Mengi yamesemwa kuhusu safu hiyo. Mimi kwa upande wangu najikita zaidi kwenye njia iliyotumika kuwapata viongozi hao na jinsi mfumo wa demokrasia unavyofinywangwa na chama ili kupata viongozi wake.
Kwanza nianze na jinsi nafasi ya mwenyekiti iliyogombea na Rais Jakaya Kikwete peke yake na tunaambiwa kuwa ameshinda kwa asilimia 99.92.
Kabla hata mkutano huo haujaanza, kulionekana vipeperushi vikimtaka Rais Kikwete asigombee nafasi hiyo kwa maelezo kuwa ingekuwa vyema apunguziwe majukumu kwa kutomhusisha na uongozi wa chama na Serikali kwa wakati mmoja.
Hata hivyo, kwa kuliona hilo, mikakati iliwekwa ili kundi linaloonekana kumpinga mwenyekiti lidhibitiwe.
Hata ilipofika siku ya uchaguzi, ilibidi Katibu Mkuu wa zamani, Yusuf  Makamba aalikwe jukwaani kueleza umuhimu wa kuendelea na uenyekiti wa Rais Kikwete.
Makamba kama kawaida yake akitumia Biblia na Qur’an alimnadi vyema Rais Kikwete huku akivuna sifa nyingi kutoka kwa makada wa chama hicho na kutumia nafasi hiyo kulaani walioandaa mpango huo ulioitwa ‘kura za maruhani’.
Wakati wa uchaguzi, utaratibu mpya uliwekwa ambapo wajumbe sasa walitakiwa kupiga kura kwa mikoa yao. Ili ikitokea mkoa fulani umempinga Rais Kikwete basi wajue namna ya kuufinya huko baadaye.
Njia zote hizo ziliwafanya watu wenye mawazo mbadala, kunywea na kulazimika kupiga kura zote kwa Rais Kikwete.
Haikuwa rahisi kupata asilimia 99.92, ilibidi mikakati ifanyike kama hivyo. Hivyo hivyo kwa makamu wenyeviti yaani Philip Mangula na Dk Ali Mohamed Shein waliopata asilimia 100. Unaambiwa hakuna hata kura moja iliyoharibika.
Kwa kweli hii ‘ni demokrasia iliyovuka mipaka ya kimataifa’. Yaani ndiyo kusema kuwa ndani ya CCM hakuna mawazo mbadala? Au hakuna watu wanaotaka fulani awe mwenyekiti badala ya Rais Kikwete au makamu wake Dk Shein, au Mangula?
Mimi siamini, maana yake ni kama vile kura zilipigwa na ‘robot’. Siamini kwa sababu kwanza tangu awali kulikuwa na vipeperushi vikiwashawishi wajumbe kutomchagua Rais Kikwete bali mtu mwingine, japo hatajwi.
Vilevile kutokana na mikakati iliyowekwa katika uchaguzi huo nayo inaleta mashaka.
Ndiyo kusema safu hiyo iliyowekwa CCM ilikuwa ya kimkakati na ilihitaji tu baraka za wanachama.
Utaratibu huu wa kusimamisha mtu mmoja kugombea bila kuwepo mtu wa pili wa kumshindanisha naye ndiyo ule uliokuwa ukitumiwa na Mwalimu Nyerere baada ya kuvunja vyama vya upinzani mwaka 1965.
Pamoja na mema mengi aliyofanya Mwalimu Nyerere, ukweli ni kwamba hakupenda upinzani wala mawazo mbadala. Ndiyo maana katika chaguzi zote ziwe ndani ya chama au uchaguzi mkuu aligombea yeye peke yake na kivuli hadi alipong’atuka mwaka 1985.
Kwake ilikuwa ni ‘zidumu fikra za mwenyekiti wa chama’.  Huo ndiyo utamaduni unaoendelea ndani ya CCM, hata kama wanachama hawamtaki mwenyekiti basi demokrasia inafinyangwafinyangwa huku ikitiliwa maneno matamu ya kina Makamba, ndipo mwenyekiti anapatikana.
Hakuna ushindani wa kweli, hakuna uwazi, hakuna usawa.
Hili haliko CCM tu, hata baadhi ya vyama vya upianzani mambo ni hayo hayo, viongozi wameshawekwa, halafu usanii tu unafanywa ili kuwapitisha.
Kuna baadhi ya vyama vya siasa, tangu vilipoanzishwa mwanzoni mwa miaka ya 1990, viongozi ni wale wale miaka nenda rudi.
Lakini kwa kuwa CCM ni chama kikongwe, basi kingepaswa kutoa somo le demokrasia kwa vyama vingine.
Vyama vya siasa vinapaswa kuonyesha demokrasia ya kweli ndani yao kabla ya kwenda kushindana na vyama vingine. Kama viongozi wa vyama watavumilia kushindwa ndani ya vyama hivyo basi watajenga utamaduni wa kuvumilia hata matokeo ya uchaguzi mkuu. Ila kama hayo yanashindikana ndani ya vyama, pia ni ndoto kuwa na demokrasia ya kweli nchini.
Elias Msuya ni mwandishi wa makala wa gazeti la Mwananchi; 0754 897 287

No comments:

Post a Comment

Ji husishe kwa maoni yako ndio ukweli upatikane kwa manufaa wetu